Visababishi
Mara nyingi maambukizi ya mfumo wa mkojo husababishwa na bakteria ambao hupanda kupitia mrija wa mkojo (urethra) kwenda kwenye kibofu. Wakati mwingine hupanda juu zaidi na kwenda kwenye figo. Wakati mwingine virusi au fangasi huweza kusababisha hali hii. Hii hutokea zaidi kwa watu wenye upungufu wa kinga ya mwili. 2
Vihatarishi
Wanawake wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi haya kuliko wanaume. Hii ni kwa sababu ya ukaribu wa njia ya mkojo na njia ya haja kubwa pamoja ufupi wa urethra, mrija unaotoa mkojo nje ya mwili. Sababu nyingine zinazowaweka wanawake kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya mfumo wa mkojo ni:
- Ujauzito
- Kujamiiana, hii huweza kusaidia bakteria au vimelea vingine vilivyopo kwenye njia ya haja kubwa kusogea karibu na njia ya mkojo
- Mabadiliko ya homoni baada ya hedhi kukoma.
Wanaume pia huweza kupata maambukizi ya mfumo wa mkojo. Vihatarashi kwa wanaume ni pamoja na hali zinazosababisha kuziba kwa njia ya mkojo ikiwemo kuvimba kwa tezi dume. Watoto wachanga ambao hawajatahiriwa pia huweza kupata hali hii kirahisi. 3
Kuwa na udhaifu wa mfumo wa kinga ya mwili, kutumia mipira ya mkojo na kisukari humuweka mtu kwenye hatari ya kupata maambukizi haya. 4
Dalili za UTI
Dalili za maambukizi ya njia ya mkojo (dalili za UTI) zinatofautiana baina ya mtu na mtu. Pia dalili hutegemea na sehemu ya mfumo wa njia ya mkojo iliyoathirika.
Dalili za kawaida za maambukizi ya sehemu ya chini ya mfumo wa mkojo ni pamoja na: 5
- maumivu wakati wa kukojoa,
- kukojoa mara kwa mara,
- maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo
- Kukojoa mkojo wenye harufu kali,
- Damu kwenye mkojo ingawa hii hutokea mara chache
Dalili za kawaida za maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo wa mkojo: 6
- Homa,
- Kuhisi baridi,
- Kujihisi vibaya.
- Maumivu katika sehemu ya ubavu au mgongo huweza kuashiria kuwa maambukizi yamesambaa kwenye figo.


0 Comments